Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki (kulia) akimsikiliza Makamu mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam,

Prof Rwekaza Mkandala(kushoto) nje ya  ukumbi wa Nkurumah kwa kabla ya  ufunguzi wa semina ya Kataa uhalifu iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya jeshi la Polisi na Chuo kikuu cha Dare s Salaam.katikati  ni Mkuu wa Shule ya Sheria Prof.Hamudi Majamba 

Watakiwa kuuchukia uhalifu kwa vitendo

Wananchi wametakiwa kuuchukia uhalifu kwa vitendo pamoja na kuwa na kauli moja katika kupambana nao kwa kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kukomesha vitendo hivyo hapa nchini.

Hayo yalisemwa jana  na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki wakati alipokuwa akifungua semina ya siku moja katika ukumbi wa Nkurumah iliyokuwa na kauli mbiu ya Kataa uhalifu iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Jeshi la Polisi na Shule kuu ya Sheria ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kupambana na uhalifu hapa nchini, semina ambayo iliwashirikisha wahadhiri, maofisa wa Polisi na wanafunzi wa chuo hicho.

Kaniki alisema wananchi wakiukataa uhalifu watawezesha jamii ya watanzania kuwa salama na kuondoa vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa uhalifu ndio kikwazo katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Aidha aliwaomba wasomi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam hususani wanaosomea shahada ya sanaa katika utekelezaji wa sheria kufanya tafiti ambazo zitaweza kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutatua kero za uhalifu hapa nchini.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof.Rwekaza Mukandala alisema jukumu la kupambana na uhalifu sio la jeshi la polisi pekee bali ni jukumu la watu wote.

Aliongeza kuwa  kwakutambua hilo mwaka 2009 walianzisha shahada ya utekelezaji wa sheria ambayo asilimia kubwa ya wanafunzi wanatoka katika vyombo vya ulinzi na usalama na wakufunzi wa shahada hiyo ni maofisa  kutoka katika Jeshi la Polisi.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Diwani Athuman alisema kauli mbiu hiyo ya kataa uhalifu ilibuniwa na Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) ili kutimiza malengo yake ya kuwa na dunia iliyo salama  kwa binadamu ambapo kwa hapa nchini ilizinduliwa mwaka jana kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Alisema katika semina hiyo wajumbe watapata fursa ya kujadili kwa pamoja makosa yaliyopo hapa nchini yakiwemo ya madawa ya kulevya, ujangili, mauaji ya albino, mauaji ya vikongwe, kujichukulia sheria mkononi , waham,iaji haramu pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu.