Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amemaliza ziara yake ya siku 13 katika mikoa ya kanda ya ziwa  pamoja na mkoa wa Singida huku akiacha morali kwa watendaji wa Jeshi la hilo , hatua ambayo italiwezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi  katika kukabiliana na matishio ya uhalifu.


IGP Sirro  amefanya ziara hiyo ikiwa ni mkakati wake  aliojiwekea  tangu  alipoteuliwa  kuwa  mkuu wa Jeshi hilo kwa lengo la kujitambulisha, kuzungumza na askari na maofisa ili kufahamu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


Katika mazungumzo yake,  IGP Sirro  amewataka askari na maofisa kutimiza  wajibu wao kwa kutenda haki  na bila uwoga wala kumuonea mtu muhali jambo ambalo litarahisisha  upatikanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu  katika jamii.


Hata hivyo,  katika mabaraza ya askari na baadhi ya maofisa  hoja mbalimbali ziliibuliwa  kutoka kwa baadhi ya askari  aliopata nafasi ya kutoa maoni yao katika kuboresha utendaji kazi ili kuimarisha  usalama wa raia na mali zao.


Aidha,  katika ziara  yake, IGP Sirro  alipata  fursa ya kukutana  na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama za mikoa  huku masuala kadhaa ya kiusalama mbinu na mikakati  ikijadiliwa katika kamati hizo na kuahidi kutoa ushirikano  utakaowezesha kukabiliana na matishio mbalibali ya kiuhalifu.