Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohame Shein akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro alipofika Ikulu mjini Unguja kwa lengo la kujitambulisha baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa jeshi la Polisi Tanzania. Rais Shein amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuimarisha vyema amani na utulivu visiwani Zanzibar.

Rais Shein amesema, ana matumaini makubwa kwa uongozi wa IGP Sirro na alimuahidi kuwa ataendelea kushirikiana naye pamoja na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ili Jeshi hilo lizidi kupata maendeleo sambamba na kusimamia vyema amani na utulivu.

IGP Sirro ametoa shukrani kwa Dk Shein na kumpongeza kwa ushirikiano mkubwa linaoupata Jeshi la Polisi kutoka kwa wananchi na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi.

IGP alimhakikishia Rais kuwa, hatua za makusudi zitachukuliwa kuhakikisha changamoto zilizopo kwenye Jeshi la Polisi Zanzibar zitatafutiwa ufumbuzi pamoja na kusimamia amani na utulivu visiwani hapo.