Vikundi vya ulinzi shirikishi kote nchini vimetakiwa kuwa makini na kuzingatia madili katika kutekeleza majukumu yao ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kupunguza    

uhalifu hapa nchini.Hayo yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IJP Ernest Mangu wakati akijibu swali kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa program ya Polisi jamii na Ulinzi shirikishi ambapo alibainisha kuwa mpaka hivi sasa vikundi hivyo vimefikia zaidi ya 4500 nchi nzima

IJP Mangu alijibu swali hilo wakati alipokutana na waandishi wa habari wa Jeshi la Polisi ofisini kwake Makao makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es salam na kuongeza kuwa, kuongezeka vikundi hivyo ni mafanikio makubwa sana kwa Jeshi hilo kwani inaonesha jinsi gani jamii imeelewa na kutekeleza kwa vitendo dhana nzima ya ulinzi shirikishi/ Polisi jamii kwa lengo la kupunguza uhalifu katika makazi yao kwa lengo la kujiletea maendeleo bila bugudha ya uhalifu na wahalifu”
Alisema kuwa ili taifa na jamii iweze kuendelea kiuchumi ,kiutamaduni na kijamii wananchi wote kwa ujumla hatuna budi kuwekeza katika suala la ulinzi na usalama kama mtaji wetu wa maendeleo.
Vikundi hivyo vimekuwa vikisaidia katika suala la ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo wengine wamekuwa wakifanikisha kukamata na kudhibiti uhalifu na wahalifu kwa kutoa taarifa katika vituo vya Polisi na kufanya ukamataji salama.
Alisema kuwa lengo la Program hiyo ni kupunguza uhalifu na wahalifu kwenye jamii kila mtaa, kijiji, kitongoji hadi ngazi ya familia na kuwa daraja la kuunganisha kila familia katika kutambua viashiria vya uhalifu na uvunjifu wa amani pamoja na stadi za utatuzi wa migogoro ndani ya jamii.
IJP Mangu aliongeza kuwa, hatua hiyo imesaidia sana katika kuwajengea uelewa wananchi juu ya kutambua na kubaini viashiria vya uhalifu na wahalifu na kuweza kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi za kuwepo kwa viashiria vyovyote vyenye lengo la kuhatarisha amani ama kuharibu amani iliyopo hapa nchini.
Moja ya kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi nchini ni utekelezaji wa program ya maboresho ambayo inalenga kuwa na Jeshi dogo la kisasa, lenye weledi na linaloshirikisha jamii katika masuala ya ulinzi, Ushirikiano huo wa wananchi lengo lake kubwa ni kudhibiti vitendo vya uhalifu na kutekeleza dira ya taifa ya maendeleo 2025 inayoelekeza kuwepo kwa utawala bora na uwajibikaji.
Pia alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa uhalifu na uvunjifu wa amani mapema katika vituo vya Polisi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahalifu kwani hiyo pia ni moja ya mbinu ya kudhibiti wahalifu katika jamii.
Mbali na mwito huo pia aliwataka watendaji wa Serikali za vijiji, mtaa wakuu wa tarafa na wilaya, viongozi wa dini na kisiasa pamoja na kamati zote za ulinzi na usalama katika ngazi zote kuanzia kitongoji, kijiji, mtaa hadi mkoa kutumia fursa hiyo itakayosaidia kubaini migogoro, matatizo/kero za jamii mapema na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati kabla ya madhara kutokea.