SHELUI WAOMBA GARI NA ASKARI POLISI KUDHIBITI AJALI

SINGIDA ALHAMISI MACHI 04, 2010.

Wananchi wa tarafa ya Shelui, katika Wilaya Iramba Mkoani Singida, wamemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuongezewa askari na kuwapatia gari la Kituo cha Polisi Shelui ili kusaidia kupunguza uhalifu ukiwemo wa ajali za barabarani.

Wananchi hao wamesema kuwa askari Polisi wa kituo cha Shelui wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wa usafiri katika kukabiliana na matukio ya uhalifu hasa wa ajali zinazotokea mara kwa mara katika eneo la mlima wa Sekenke, mlima ambao una historia ya kutokea ajali mbaya za mara kwa mara.

Ajali katika eneo la mlima huo wenye kona nyingi na miamba zimekua zikisababisha vifo vya watu wengi na wengine kuachwa wakiwa na vilema vya kudumu na upotevu ama uharibifu wa mali.

Wananchi hao walikuwa wakizungumza wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi alipotembelea Shelui kuona maendeleo ya ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi cha kata hiyo kinachojengwa kwa nguvu za wananchi.

Hadi sasa ujenzi wa Kituo hicho umengarimu zaidi ya shilingi milioni 8 na inakaridiwa hadi kumalizika kabisa kituo hicho kitakuwa kimegharimu jumla ya shilingi milioni 16.

Akizungumza na Wananchi hao, IGP Mwema alisema kuwa Serikali inathamini sana michango ya wananchi wakiwemo wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya Polisi na nyumba za askari.

Kutokana na uwezo mdogo uliopo kwa wananchi wa Kata hiyo katika kuchangia ujenzi wa kituo hicho, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Mwema, amechangia kiasi cha shilingi milioni tano ili kuunga mkono nguvu za wananchi.

IGP Mwema amepongeza juhudi hizo na kuwaomba wananchi wa maeneo mengine kufikiri na kutenda kama wenye mali kwa kuangalia vipaumbele na hata kuchangia ujenzi wa vituo vya Polisi na huduma nyingine za Jamii kama hatua ya kujikwamua.

Akiwa njiani kuelekea wilayani Iramba, Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini amesimama kwa muda katika kituo kidogo cha polisi cha Misigiri ambapo alipata maelezo ya utendaji kazi katika kuzuia ajali za barabarani unaofanywa kwa pamoja na askari Polisi kutoka vitengo mbalimbali.

Mkuu wa kituo hicho cha Polisi Sajenti James Kessy, alimwambia IGP Mwema kuwa, mpango wa kufanya kazi kama timu umefanikisha kupunguza matukio ya ajali na malalamiko ya kuomba na kupokea rushwa.

Askari hao kwa pamoja na bila kificho, wamekuwa wakiwaelimisha madereva juu ya hali ya barabara na kuwataka kuwa makini hasa wafikapo kwenye eneo la mlima wa Sekenke.

IGP Mwema pia alitembelea katika kijiji cha Kinyangili kutoa mkono wa pole kwa wananchi waliopambana na majambazi kwa kushirikiana na Polisi baada ya kupora kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wafanyabiashara mwishoni mwa mwaka jana ambapo aliahidi kutoa shilingi milioni moja kwa wahanga waliojeruhiwa wakati wa tukio hilo ambapo watu wanne wakiwemo majambazi waliuawa baada ya kumuuwa mwananchi mmoja kwa kumpiga risasi wakati wa mapambano

Mkuu huyo wa Jeshi laPolisi nchini, yupo mkoani Singida kwa ziara ya wiki moja kuangalia hali ya usalama na kuhimiza mpango wa Polisi jamii na ulinzi Shirikishi.

Mwisho

 
< Prev   Next >
Copyright 2010 Tanzania Police Force Website.