RC SINGIDA AWAPIGIA DEBE POLISI KUPATIWA MAGARI MAPYA

SINGIDA JUMANNE MACHI 02, 2010.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Bw. Paraseko Kone, amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuangalia uwezekano wa kuupatia mkoa wa Singida magari ya kutosha ili Polisi waweze kukabiliana na uhalifu kwa urasihisi.

Bw. Kone alitoa ombi hilo wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kilichohudhuriwa pia na Waziri wa Sheria na Katiba Mh. Mathias Chikawe, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidiai Mwema.

 

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini yupo katika ziara ya wiki moja ya kuutembelea mkoa wa Singida kukagua utekelezaji wa mchakato wa maboresho ya Jeshi la Polisi hapa nchini.

Bw. Kone amesema kuwa mkoa wa Singida unahitaji zaidi ya magari 20 ya Polisi lakini hivi sasa una magari sita tu na baadhi yake ni mabovu kiasi cha kutokidhi mahitaji kwa watendaji wa Jeshi hilo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amesema kutokana na miundombinu duni ya barabara za mikoa mingi hapa nchini, kuna haja ya Serikali kufikiria kupeleka magari mapya mikoani na yanapokaribia kuchoka ndipo yarudishwe mijini kwa matumizi mengine.

Amesema hali hiyo itarahisisha utendaji wa maafisa na askari waliopo katika mikoa ya pembezoni mbali ya kua ina miundombinu duni lakini pia ina matumizi ya masafa marefu tofauti na mijini ambako kuna lami na umbali mfupi wa kufanyia kazi.

Ameongeza kuwa hata mafundi wa zuri wapo mijini na hivyo itakuwa rahisi hata magari hayo yakiharibika kuyatengeneza.

 

Hata hivyo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP) Saidi Mwema, alisema Jeshi hilo linatambua uhaba wa vitendeakazi likiwemo suala la usafiri na uhaba wa makazi kwa askari.

Amesema kuwa Jeshi hilo lipo katika mpango wa maboresho na mwaka wa fedha ujao ni mwaka wa kuanza utekelezaji wa maboresho na kuanza kungalialia vipaombele katika kila mkoa ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezo wa kibajeti wa utekelezaji.

Naye Waziri wa Sheria na Katiba Mh. Chikawe, amesema kuwa Serikali imetoa madaraka mikoani ya kuajiri watumishi wa ngazi ya chini kwa Idara za mahakama ili kuondoa ucheleweshwaji wa kesi.

Amewataja watumishi wanaoweza kuajiliwa na ngazi ya mkoa kuwa ni Madereva, wapiga Chapa, makarani wa mahakama za Mwanzo na wahudumu.

Mwisho
 
< Prev   Next >
Copyright 2010 Tanzania Police Force Website.