MAKAMANDA WAAGIZWA KUKAZA BUTI KUKOMESHA UHALIFU

DODOMA ALHAMISI FEBRUARI 25, 2010. Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa linadhibiti mapema wimbi la uhalifu na kuimarisha nidhamu kwa askari kuondokana na vitendo vya rushwa.

Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu wa mambo ya Ndani Mh. Mbarak Abdullwakili, wakati akifunga mkutano wa Maafisa wakuu wa Jeshi la Polisi uliokuwa ukifanyika kwenye ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, mjini Dodoma.

Mh. Abdllwakili amesema kuwa ingawa hivi sasa wananchi wamejenga imani kubwa na Jeshi la Polisi kutokana na kujituma kwa ufanisi, lakini kama matukio ya kiuhalifu yakiendelea na kuto dhibitiwa mapema kuna hatari ya wananchi kupoteza imani kwao.

Hata hivyo amesema kuwa matukio hayo na yale ya ajali za barabarani yasiwakatishe taamaa lakini iwe ni changamoto kwa Jeshi la Polisi kujipanga upya kukabiliana na hali hiyo.

Amesema Jeshi la Polisi katika nchi yoyote ile duniani ndilo linalotoa taswira ya Taifa husika, kwa hivyo ipo haja ya Jeshi na askari mmoja mmoja kujitazama upya na kujikosoa na kumkosoa mwingine pale wanapomuona anakwenda kinyume na matarajio ya wananchi.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, amesema kuwa mkutano huo ambao ulikuwa ukiwashirikisha Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, umejadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na uhalifu ukiwemo wa vitendo vya kudai na kupokea rushwa.

Amesema kuwa pamoja na mambo mengine, makamanda hao kwa ujumla wao, wameahidi kwenda kuwasimamia kwa karibu askari waliochini yao na kujiona kama wao ni wenye mali.

Amesema Makamanda hao pia watahakikisha kuwa kila askari anafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki za binadamu kwa lengo la kuepuka malalamiko lakini pia kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayemuonea mwingine bila ya kuchukuliwa hatua.

Akizungumzia matarajio ya Taifa kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu, IGP Mwema amewaondolea hofu wananchi kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa wa huru na wa haki.

IGP Mwema ametumia nafasi hiyo kuwaomba wanasiasa kutokua chanzo cha vurugu na ghasia na kwamba kwa jeshi la Polis, kila mmoja atapata haki sawa kiusalama bila ya upeleleo.

Pamoja na mambo mengine, Makamanda hao wametoa maazimio 15 yakiwemo ya kuahidi kutoa elimu kwa wamiliki binafsi wa mbwa na farasi ili watumike kama walinzi wasaidizi na.

Aidha wamesema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kwa wananchi hasa katika wakati huu wa utandawazi, watahakikisha kuwa wanatoa ushirikiano wa karibu utakaowawezesha waandishi kuhafanya kazi zao kwa uhuru.

Mwisho

 
< Prev   Next >
Copyright 2010 Tanzania Police Force Website.