POLISI KAGERA WAUA MAJAMBAZI WAWILI NA KUPATA SMG 2 NA MABOMU YA MKONO

NGARA KAGERA DESEMBA 22, 2009. Polisi mkoani Kagera wameyaua majambazi mawili kwa kuyapiga risari katika mapambano makali na kufanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG, risasi 62 na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera ACP Henry Salewi, amesema kuwa tukio hilo limetokea leo 22/12/09 alfajiri huko kwenye Pori la Mjerumani karibu na kijiji cha Bugalama wilayani Ngara wakati Polisi walipokuwa kwenye doria ya kudhibiti ujambazi wa kuteka magari kwenye pori hilo.

 

Kamanda Salewi amesema Askari hao wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ngara mkoani humo, SP Mohammed Milanzi na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa huo SP Peter Matagi, waliwaona watu wanne kati yao watatu wakiwa na silaha aina ya SMG na mmoja akiwa na begi lililokua na mabomu matatu ya kutupwa kwa mkono pamoja na magazine iliyokuwa na risasi 30.

 

Hata hivyo Kamanda Salewi, amesema kuwa wakati wa mashambulizi hayo, majambazi wawili walifanikiwa kutoroka wakiwa na silaha moja aina ya SMG.

 

Kamanda Salewi amesema kuwa Polisi inaendelea kuwasiliana na wananchi mbalimbali ili kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Ngara kwa ajili ya kufanya utambuzi wa majambazi hayo.

 

Amesema Makachero wa Polisi mkoani humo wanaendelea kufuatilia taarifa ya kuyapata majambazi yaliyotoroka na kwamba amewataka wananchi kutoa taarifa Polisi kama watawaona watu wawili wakiwa na majeraha wakitafuta tiba ili wakamatwe.

 

Hivi karibuni Polisi mkoani humo waliyaua kwa risasi majambazi nane katika matukio mawili tofauti yaliyotokea wilayani Biharamulo na kufanikiwa kupata silaha saba aina ya SMG na risasi 607 na mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono.

Mwisho
 
< Prev   Next >
Copyright 2010 Tanzania Police Force Website.