WATOTO WATATU WAFA MAJI

SUMBAWANGA RUKWA, JUMAMOSI NOVEMBA 28, 2009.Watoto watatu wa familiya moja wakiwemo mapacha wawili kwenye kijiji cha Kisumba katika wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye shimo la choo lililojaa maji nje ya nyumba yao.

 
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Jacobo Mwaruanda amewataja watoto waliofariki kuwa ni mapacha wakike RESTUTA WASULWA na HELENA WASULWA wote wakiwa na umri wa mika mmoja pamoja na kaka DERICK WASULWA(3).
 
Amesema kuwa siku ya tukio hilo juzi majira ya saa 2:00 asubuhi wakati wazazi wao wakiwa hawapo nyumbani na watoto hao waliamka na kuanza kuchezea maji kwenye shimo hilo na ndipo walitumbukia na kufariki dunia.
 
Kamanda huyo amesema kuwa shimo hilo ambalo lilikuwa na kina cha futi nane lilichimbwa na Bw. Bartazary Wasulwa (22), ambaye ni baba wa marehemu hao kwa ajili ya choo.
 
Amesema kabla ya choo hicho kujengewa ndipo shimo hilo lilipojaa maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
 
Amesema siku ya tukio hilo wazazi wote walikuwa hawapo nyumbani na walitoka kuelekea katika shughuli mbalimbali na watoto hao waliachwa wakiwa bado wamelala.
 
Kamanda amesema kuwa mama yao aliporejea nyumbani majira ya saa 2 asubuhi, aliikuta miili ya watoto hao ikielea majini wakiwa wamesha fariki dunia.
 
Uchunguzi wa daktari umebainisha kuwa vifo hivyo vilitokana na kunywa maji mengi na kukosa kosa hewa baada ya kuzama majini.
 
Kaimu Kamanda huyo ametoa rai kwa wananchi mbalimbali kutoyaacha wazi mashimo ya vyoo ama yaliyochimbwa kwa ajili ya udongo wa kujengea ili kuepuka majanga kama hayo.
 
Mwisho

 

 
< Prev   Next >
Copyright 2010 Tanzania Police Force Website.