Main Menu
Useful Links
| Tahadhari za Usalama |
| Polisi Jamii |
| Vifungu vya Sheria |
| SMS & CALLS |
Who's Online
We have 9 guests onlineLogin Form
Kikosi cha Usalama Barabarani
|
HISTORIA YA KIKOSI: Kuundwa kwa Kikosi: Kikosi cha Usalama Barabarani kiliundwa rasmi mwaka 1976. Kabla ya hapo shughuli za usalama barabarani zilifanywa moja kwa moja chini ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa. Mabadiliko hayo ya Kimuundo yalilenga zaidi katika kuleta ufanisi wa shughuli za kusimamia suala zima la usalama barabarani nchini. Chini ya muundo mpya, majukumu yote yanayohusiana na Sera za Usalama Barabarani yalihamishiwa Kikosini, na Makamanda wa Mikoa walibaki na majukumu yanayohusiana na utendaji na utawala.
Uongozi wa Kikosi:
Tangu kuundwa kwake mwaka 1976, Kikosi kimeongozwa na jumla ya Makamanda tisa hadi sasa. Kamanda wa kwanza wa Kikosi alikuwa Kamishina Msadizi Emson Mkisi ambaye kwa sasa amestaafu, na alifuatiwa na Kamishina Msaidizi Mwandamizi William D?vaz ambaye aliacha nafasi hiyo kwa kustaafu kazi ya Upolisi na sasa ni marehemu. Baadaye alifuata Kamishina Msadizi Bazo Shiyo ambaye amestaafu kwa sasa. Kamanda wa nne alikuwa Kamishina Msaidizi Mwandamizi Elphas Saanya ambaye alistaafu mwaka 1999 na kumwachia Ukamanda Kamishina Msaidizi Luther Mbuttu, sasa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. Baada ya kutoka Kamishina Msaidizi Mbuttu ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam aliteuliwa Kamishina Msaidizi Leonard Mashaka kuwa Kamanda wa Kikosi ambaye kwa sasa amehamishiwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai. Mwaka 2003 Kamishina Msaidizi Mwandamizi Eshifyoose Mosha aliteuliwa kukiongoza Kikosi hadi Februari, 2005 alipostaafu. Baada ya kustaafu aliteuliwa Kamishina Msaidizi Mwandamizi Peter L. Kivuyo ambaye alichukua nafasi ya Kamishina Msaidizi Mwandamizi Eshifyoose Mosha akiwa anatokea Mkoa wa Pwani ambako alikuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo. Hivi sasa Kamanda Kivuyo amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi. Kikosi kinaongozwa na Kamishina Msaidizi Mwandamizi Peter L. Kivuyo ambaye alichukua nafasi ya Kamishina Msaidizi Mwandamizi Eshifyoose Mosha akiwa anatokea Mkoa wa Pwani ambako alikuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo. Kwa hivi sasa Kikosi hiki kinaongozwa na Kamishna Msaidizi Mselem Mtulia.
Mabadilliko ya Vitendea kazi:
Kutokana na madiliko ya Teknolojia, Kikosi cha Usalama Barabarani kimepitia katika hatua mbali mbali kwa upande wa vitendea kazi. Tofauti na ilivyo sasa ambapo Askari wanaoongoza Misafara kwa kutumia Pikipiki kubwa aina ya Honda zenye uwezo wa kwenda mwendo kasi hadi Kilometa 240 kwa saa, kipindi mara baada ya Uhuru Askari waliongoza Misafara kwa kutumia Pikipiki aina ya Triumph kutoka Uingereza. Baadaye zilianza kutumika Pikipiki aina ya Honda zenye ukubwa wa Injini wa Sentimeta za ujazo (cc) 350 na 360, na Yamaha zenye ukubwa wa Injini wa (cc) 350. Kisha zilianza kutumika Honda zenye ukubwa wa Injini (cc) 550 na 650, ambapo sasa zinatumika Honda zenye ukubwa wa Injini (cc) 750.
Aidha, Kwa upande wa magari, misafara ya viongozi mara baada ya uhuru iliongozwa kwa kutumia magari aina ya Cortina yaliyofuatiwa na magari aina ya Peugeot 404 na baadae Peugeot 504. Kwa sasa yanatumika magari aina Mercedes Benz, Hyundai na Land Rover Discovery.
Katika jitihada za kuongeza ufanisi, mwaka 1995 Kikosi kilianza kutumia Kompyuta kwa ajili ya kuweka na kuchambua kumbukumbu za ajali. Kwa sasa Mikoa nane inatumia Kompyuta kwa ajili ya kazi hiyo na jitihada zinafanywa ili Mikoa mingine yote iweze kupata Kompyuta.
Kwa upande wa mavazi, Askari wa Usalama Barabarani wa Vyeo vya kuanzia Stafu Sajenti kurudi chini walianza kuvaa Sare nyeupe mwaka 1980. Kabla ya hapo, Askari walikuwa wakivaa nguo za Khaki (Tunic), Mkanda (Cross Belt) na Kofia nyeupe. Kwa upande wa mavazi ya Sherehe (Ceremonial Dress) Askari waendesha Pikipiki (Riders) walikuwa wakivaa Shati nyeupe na Tai, Khaki nyeupe Koti pamoja na Suruali tofauti na sasa ambapo wanavaa Makoti meupe pamoja na Suruali za bluu
Mabadiliko ya Sheria: Kikosi kinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani Na.30 ya mwaka 1973 ambayo ndiyo Sheria Mama. Sheria hii, ambayo matumizi yake yalianza tarehe 1 Januari 1974, iliifuta Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 (Traffic Ordinance CAP.168) ambayo ilikuwa inatumika hapo awali. Hata hivyo, baadhi ya Kanuni zilizotokana na Sheria ya Usalama Barabarani bado zinaendelea kutumika hadi sasa na baadhi zimefutwa katika vipindi tofauti baada matumizi ya Sheria Na.30 ya mwaka 1973 kuanza.
Kama zilivyo sheria nyingine, Sheria ya Usalama Barabarani Na.30 ya mwaka 1973 imefanyiwa marekebisho mbali mbali. Marekebisho hayo ni kama yale yaliyofanyika mwaka 1980 kwenye Sheria ya Usalama Barabarani Na.15 na kutamka bayana kuwa dereva anayetumia gari kufanya uhalifu leseni yake ifutwe na kuwa gari linalohusika na shughuli hiyo litaifishwe endapo Mmiliki wake atakuwa ameruhusu litumike kwa kazi hiyo. Mwaka 1990 Sheria ya Usalama Barabarani ilirekebishwa kwa Sheria Na.4, ambayo pamoja na mambo mengine, ilianzisha upimaji wa madereva walevi kwenye Vituo vya Polisi kwa kutumia vifaa maalum badala kuwapeleka Hospitali kutolewa damu kwa lengo la kuwapima viwango vya ulevi. Halikadhalika Sheria ya Usalama Barabarani ilirekebishwa mwaka 1996 kwa Sheria Na.16, ambayo ilipandisha viwango mbali mbali vya adhabu, na kuanzisha ufungaji wa vidhibiti mwendo kwenye mabasi ya abiria. Na mwaka 2000, chini ya Kanuni za Mashitaka bila kufikishwa Mahakamani (The Road Traffic – Nofication of Offences- Regulations, 2000) zilizotolewa na Gazeti la Serikali Na.249 la Tarehe 30 Juni 2000, adhabu kutokana na makosa yanayohusiana na utaratibu huu zilianza kulipiwa kwenye Vituo vya Polisi badala ya Mahakamani kama ilivyokuwa hapo awali.
Mbali na Sheria ya Usalama Barabarani, Kikosi cha Usalama Barabarani husimamia Sheria ya Shule za Udereva Na.14 ya mwaka 1965. Sheria hiyo inampa Mamlaka Inspekta Jenerali wa Polisi kumteua Msajili wa Shule na Wakufunzi wa Udereva. Kwenye Kanuni zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na.529 la Tarehe 02.07.1983, Inspekta Jenerali wa Polisi alimteua Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa Msajili ambaye anafanya kazi hiyo hadi sasa. |
|
|
|